Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema walikuwa na wazo la kuishirikisha Yanga katika mashindano yao ya wiki moja ya ‘Simba Super Cup’.
Mashindano hayo ya Simba yanayoshirikisha timu tatu pekee yanatarajiwa kuanza kesho kwa wenyeji kuwaalika TP Mazembe, kabla ya wageni hao kucheza na Al Hilal na kisha kumaliza na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Barbara alisema walikuwa na wazo la kuwashirikisha mahasimu wao hao, Yanga katika michezo hiyo, lakini baada ya majadiliano ya kama watakubali au la, wakaamua kuahirisha.
Kiongozi huyo wa juu wa Simba alisema wazo hilo lilikuwa kwa nia njema, kwani kwao hawakuwa wakihitaji kuonyeshana ubabe kwa upinzani walionao, bali kutumia kama njia mojawapo ya kujiandaa kimataifa.“Ni kweli, tulikuwa na wazo la kuiandikia barua kabisa Yanga kushiriki Super Cup, lakini tulifikiria mara mbili kama wanaweza kutujibu na kushiriki kwa wakti huu, ama wataelewa vinginevyo.
“Baada ya majadiliano ya muda tukaona tuliahirishe wazo hilo hadi wakati mwingine. Tunataka kufanya mashindano haya kufanyika kila mwaka na inawezekana kabisa wakati mwingine tukawaandikia wenzetu wa Yanga kushiriki,” alisema Gonzalez.
Simba inashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na imeanza mazoezi juzi kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili lakini pia mashindano hayo ya kimataifa mwezi ujao.
Mashindano ya Simba Super Cup yanashirikisha timu za wenyeji Simba (Tanzania), TP Mazembe (DR Congo) na A Hilal ya Sudan.
Katika mchezo wa kwanza, Simba itacheza na Al Hilal leo saa 11 jioni na kumaliza na TP Mazembe Januari 31.
Katika mchezo wao wa ufunguzi Simba, mgeni rasmi atakuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam, Omari Mutalanga.