JINA la straika wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi (30) lilikuwa linatamba kwa wadau wa soka nchini, baada ya kusajili ndani ya kikosi hicho msimu wa 2012/14, je unajua siri yake? Msikie mwenyewe anachosema.
Bahanuzi mwenye asili ya Rwanda anasema jina Bahanuzi kinyarwanda lina maana ya mtu mkubwa katika jamii, anasisitiza hakushangazwa na kuvuma ghafla alipotua Yanga.
“Mimi ni mchanganyiko, mama ni Msukuma na baba ni Mnyarwanda, licha ya Yanga kunitambulisha kwa jamii, ila hata mtaani nilikuwa nikicheza basi nakuwa maarufu vile vile,” anasema.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Bahanuzi anafunguka vitu vingi ikiwemo sababu ya kukaa nje ya soka, ndoa ilivyomtenganisha na watoto wake na anajikuta anaishi kama mkiwa kwa kila kitu kwenda ndivyo sivyo.
“Maisha ni safari ndefu, nimepitia mengi yanayoumiza moyo wangu na watu wanaonizungumzia kila wanachoweza hawanijui, wakati mwingine naona taarifa zangu kwenye mitandao ya kijamii nabakia nashangaa tu na kushukuru Mungu, nikiamini ipo siku ukweli wote wataujua,” anasema.
Kupitia gazeti lako pendwa la Mwanaspoti, utayajua mengi ambayo mchezaji huyo anayazungumza kuhusu soka na maisha yake binafsi, yalivyofanyika mwiba kwenye maisha yake.
MAISHA NDANI YA YANGA
Yanga ilimsajili Bahanunzi msimu wa 2012/14 akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, anaeleza awali alikuwa muoga kutokana na ukubwa wa klabu hasa kwa upande wa mashabiki namna walivyokuwa wanamchukulia kwa ukubwa, uliomfanya awaze mara mbilimbili jinsi ya kufanya kinachotarajiwa kwake.
Anasema baada ya muda mfupi alizoeana na wachezaji aliowakuta klabuni hapo na kwamba ilimuongezea kujiamini na akawa anafunga kwa fujo mechi za kirafiki ambazo Yanga ilikuwa inacheza kujiandaa na msimu mpya.
“Nilianza kuonekana rasmi kwenye mechi za mashindano hasa Kombe la Kagame na mechi yangu ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Vital’O ya Burundi, niliingia dakika ya 78, tulishinda mabao 2-0, mechi zilizofuata zote nilianza na kucheza dakika 90 na nilikuwa nafunga ,” anasema Bahanunzi na anaongeza kuwa,
“Mashindano ya Kagame ndio yalioling’arisha jina langu, nakumbuka niliibuka mfungaji bora, baadae ikafuata mechi ya ngao ya jamii, kisha tukaingia kucheza Ligi Kuu Bara, ikawa mwanzo mwingine wa maisha yangu kubadilika taratibu, kutoka kwenye furaha na kuingia kwenye huzuni iliyokuwa imebakia moyoni,”anasema.
Anaendelea kusimulia kuwa majukumu ya Ligi Kuu Bara, yalianza ambapo alicheza mechi tatu bila kufunga bao, hapo kasheshe ilimpata hadi kufikia hatua ya kuitwa na viongozi wake, makao makuu ya klabu yaliopo Jangwani, Dar es Salaam.
“Maneno yalikuwa mengi yaliyonizidi uwezo na umri wangu, nakumbuka niliitwa na viongozi wa Yanga wakaniuliza kwanini hufungi? Niliwajibu ligi ndio imeanza 2013/14, ajabu wakaniambia umeanza starehe za wanawake ndizo zinakutoa kwenye reli, ilinishitua na kuniumiza, ilinibidi ninyamaze kwa kuwaheshimu,” anasema na kuongeza kuwa,
“Kilichoendelea nikawa sipangwi kwenye mechi, huku tetesi za kuniita malaya zikiwa zinazidi kuendelea zaidi hadi kufikia hatua ya mke wangu kujisikia vibaya na kuwa mwenye wivu ambao ulinikosesha madili mengi ya matangazo, akidhani ndio ningepotea zaidi,” anasema.
PENALTI ILIMUONDOA
KWENYE RELI
Anakiri kwamba mwaka 2014, kitendo chake cha kukosa penalti ya ushindi dhidi ya Al Ahly ya Misri, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kilichangia kumuondoa kwenye ndoto za kufika mbali.
“Penalti ilizua nongwa, wakati bado nipo Misri nilipigiwa simu mashabiki wamekwenda kufanya fujo nyumbani kwangu, huku wakitukana matusi ya kila aina, mke na watoto walikuwa ndani na kama haitoshi wakati tunarudi hakuna mchezaji aliyekuwa ananiongelesha, kali zaidi ni matusi niliyopokewa nayo Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julias Nyerere, nikanyamaza kimya nakuomba Mungu tu,” anasema na anaongeza kuwa,
“Nilijihisi mkosaji nisiyestahili kusamehewa, roho ya kuacha soka ilinivaa, aliyenisaidia ni kiongozi, Hussein Ndama alinikalisha chini, akanijenga na kuniambia haikuwa ridhiki yako, himili mtikisiko unaokupata, nakumbuka siku hiyo alinipa dolla 500, kwani aliona jinsi wenzangu walivyokuwa wanapewa pesa na mashabiki halafu mimi nilinyimwa,” anasema.
Anaendelea kusimulia kuwa siku ya pili wakati wachezaji wenzake wanaogopa kwenda mazoezini ambayo yalifanyika Uwanja wa Kaunda, uliopo makao makuu ya klabu hiyo, aliamua kuwahi mapema 9:00 jioni na muda sahihi wa kuanza ilikuwa ni saa 10:00.
“Siku hiyo mashabiki walijaa mapema sana, baada ya kufika wachezaji wenzangu, kuna shabiki aliniita nitoke uwanjani, nikatoka kisha akanipeleka katikati ya mashabiki, akawauliza huyo anaitwa nani, wakaitikia ‘Bahanuzi’, hapo mwili wangu ulikuwa unavuja jasho huku nasikia ubaridi wa ajabu,” anaongeza,
“Akawauliza tena tumsamehe ama tusimsamehe, wakajibu tumemsamehe, baadae wakanipa maneno, wakuniambia nipunguze wanawake, ilinibidi kuwa mpole kwasababu nilikosa penalti, kisha wakaniambia haya nenda kaendelee na mazoezi, nikaenda kujiunga na wenzangu, huku moyo wangu ukijaa unyonge kuona nabaguliwa,” anasema.
Anasema penalti hiyo ni kama ilimtia nuksi, kwani hakubahatika kupangwa mpaka alipokuja kocha Mbrazil Marcio Maximo, aliyemkalisha kitako na kumwambia jinsi anavyotuhumiwa kuhusu penalti na wanawake.
“Jambo kubwa aliniambia nimeambiwa wewe unahangaika sana na wanawake, umesahau kazi yako, lakini ulikosa penalti, nakutia moyo hata mimi niliwahi kukosa uwanja mkubwa wa Brazil mara tano, soka lipo tofauti na siasa zao, piga mazoezi nione kipaji chako wanachokisema kinafifishwa na wanawake,” anasema na anaongeza,
“Alipenda nilivyokuwa nayafanya mazoezi akanipa nicheze mechi iliyofuata kila mtu akabaki anashangaa na akasema inabidi nipuuzie kinachosemwa na mashabiki na viongozi kuhusu tuhuma nilizokuwa napewa, mpaka wakamwambia nina mwanamke mnene aliyenizidi kila kitu,”anasema.
Anasema bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwani Maximo baadae alimwambia atakuwa straika namba tatu wa kwanza akiwa ni Jerry Tegete na wa pili, Gerson Jaja ambaye alitoka naye Brazil kwa lugha nyingine ni kwamba angekuwa anakaa jukwaani kushuhudia wenzake wakifanya kazi.
“Nilivyoona hivyo nikamuomba kocha niende kwa mkopo kwani tayari, Polisi Moro walikuwa wanahitaji huduma yangu, niliiona hiyo ni fursa ya kujipanga kwa kucheza muda mrefu, ambako nilijengeka kuwa fiti na akili ilikuwa inawaza kazi badala ya maneno,”anasema na anaendelea kusimulia,
“Muda ambao nilicheza Polisi Moro, nilichukua zawadi ya mchezaji bora mara mbili ya mwezi, kuhusu zawadi za hapa na pale zilikuwa nyingi, ikiwemo simu janja niliyopewa na mtu kama moja ya kufurahia kazi yangu,”anasema.
Ukiachana na furaha yake ya kucheza Moro, anasema alimkuta kocha Mohammed Rishard ‘Adolf’ akiwa kocha wa timu hiyo, anaeleza ndiye aliyemjenga na kumwambia afanye kazi bila kuangalia ukubwa wa timu, aliyotoka bali afahamike kwa kiwango kizuri.
“Ni kocha ambaye anajua kufundisha mbinu, angalia timu anazofundisha akifungwa ni bao moja tena kwa shida, hicho kitu nilikiona wakati nipo Polisi Moro,” anasema na anaongeza kuwa,
“Ni kweli Yanga walinipangia nyumba ya kifahari ila nilikuwa nakosa usingizi, tofauti na maisha ambayo niliishi Polisi Moro, ambako licha ya kuishi sehemu ya kawaida, lakini nilikuwa na furaha ambayo akili yangu ilikuwa inawaza kazi na sio maneno,”anasema.
Mbali na penalti kumuondoa kwenye reli, anakiri kwamba utoto pia ulichangia kwasababu kila kitu alikuwa anakiweka wazi, huku wenzake wakivitumia kama fimbo ya kumuumiza kuhakikisha hafanikiwi kwa njia yoyote ile.
“Nakumbuka kuna mchezaji aliniambia Said, ukitaka kuendelea kucheza Yanga nenda kwa mganga wa kienyeji, lasivyo huo utakuwa mwisho wako wa kucheza soka, lakini nilikuwa najiuliza ninakwenda kufanyaje, nilikuwa sipati jibu.”