Viongozi wa Umoja wa Ulaya leo watajaribu kutafuta mbinu za kukabiliana na aina mpya ya virusi vya corona ambayo inatishia kufungwa tena kwa mipaka ya nchi wananchama katika wakati zoezi la utoaji chanjo linakwenda kwa mwendo wa kusuasua.

Kuelekea mkutano wa kilele utakaofanyika kwa njia ya video, wakuu wa taasisi za umoja wa ulaya wamewatolea wito viongozi wa nchi wanachama kuimarisha umoja na kuongeza kasi ya kupima na kutoa chanjo dhidi ya COVID-19.
Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema kanda hiyo inapaswa kuwa imetoa chanjo kwa asilimia 70 ya watu wazima ifikapo msimu wa kiangazi na kuimarisha uwezo wake wa kubaini visa vya aina mpya ya virusi vya corona.
Zoezi la utoaji chanjo kwenye mataifa ya Umoja wa Ulaya linajikongoja huku taarifa ya kampuni ya Pfizer kuwa itapunguza kwa muda usambazaji wa dozi za chanjo imezidisha hamaki miongoni mwa mataifa ya Ulaya.