Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya wadau wa soka kuipa Simba nafasi finyu ya kupenya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kipa wa Yanga, Faruk Shikhalo ametofautiana nao akisema timu hiyo itafika mbali katika michuano hiyo kutokana na ubora wa wachezaji wake.
Baada ya ratiba ya makundi ya mashindano hayo kutoka, baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakidai kuwa huo ndio mwisho wa Simba kutokana na ubora wa timu ilizopangwa nazo.
Simba imepangwa kundi A pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, Al Merrikh ya Sudan na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na itaanzia ugenini Februari 12 kucheza na AS Vita.
Hata hivyo, Shikhalo anaamini kama Simba ikipewa sapoti na mashabiki wa soka bila kujali itikadi zao inaweza kushangaza kwenye mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Shikhalo alisema Simba ina timu nzuri yenye wachezaji wenye ubora mkubwa, hivyo anaamini itafika mbali kwenye mashindano hayo msimu huu.
“Ina wachezaji wazuri wanaoweza kuibeba timu hiyo na kuifikisha mbali kwenye hayo mashindano. Kama wataendelea kucheza hivyo kwa kujituma na ari kubwa nawatabiria makubwa.”
Shikhalo alisema Simba haipaswi kuwa na hofu licha ya watu wengi kuona kuwa wamepangwa kundi gumu kwani anaamini ikikomaa inaweza kupita hatua hiyo na kutinga robo fainali ya mashindano hayo kama ilivyofanya msimu wa 2018/2019.
“Timu zote zilizoingia hatu hiyo ni nzuri ikiwemo Simba, hivyo sioni haja ya watu kuwakatisha tamaa kuwa hawawezi kwenda zaidi ya hapo,” alisema. Kama wamefika hatua hiyo, basi wanaweza pia kwenda mbali zaidi, muhimu wapewe sapoti.”
Simba itaanzia ugenini katika hatua hiyo kuikabili AS Vita kati ya Februari 12 na 13, kisha itapambana na Al Ahly nyumbani Februari 23 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi itakayofuata wakati kati ya Machi 5-6 itacheza na Al Merrick ugenini.
Hii siyo mara ya kwanza Simba kukutana na AS Vita na Al Ahly kwani msimu wa 2018/2019 ikiwa chini ya kocha Mbelgiji Patrick Aussems ilicheza na timu hizo na kupoteza mechi zote mbili ugenini, lakini ikashinda nyumbani kwa kishindo na kutinga robo fainali ya mashindano hayo.
Ilikutana na AS Vita, Januari 19, 2019 na kulala kwa mabao 5-0, kisha ikalipa kisasi nyumbani kwa kuwachapa Wakongo hao mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Machi 16, 2019 na kufanikiwa kutinga robo fainali kwa mabao ya Mohammed Hussen ‘Tshabalala’ na Clatous Chama.
Pia, iliwahi kukutana na Al Ahly Februari 2, 2019 na kuchapwa mabao 5-0, lakini ikawafunga Waarabu hao nyumbani kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Februari 12, 2019