ACHANA na usajili wa Mnigeria, Junior Lokosa ambao tayari umeshakamilika. Mwanaspoti linajua Simba imefikia sehemu nzuri kwenye dili lake na kiungo Mmali, Moussa Kone.
Staa huyo ambaye anakipiga kwenye klabu ya Stade Malien ya nchini humo, anakuja spesho kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba iko kundi moja na Ahly ya Misri, El Merreikh ya Sudan na AS Vita ya DR Congo. Usajili wa mastaa ambao watacheza michuano ya Caf pekee unaendelea hadi Januari 31 ambapo Simba tayari imeshamalizana na Lokosa na sasa itamuongeza Kone kama mshindani wa Jonas Mkude.
Mchakato wa kutamfuta kiungo huyo ambao unaendeshwa kwa usiri mkubwa ndani ya Simba na wamepanga kuifanya kama sapraizi.
“Kone anaweza kucheza kikamilifu kama kiungo mkabaji na ushambuliaji nafasi ambayo imeonekana kuwa na upungufu hasa tunapocheza ugenini katika mashindano haya ya kimataifa,” alidokeza kiongozi mmoja wa Simba.
“Unajua usajili wa Kone na kama tutafanya mwingine ni kuweka nguvu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hawa wachezaji tutawapa mikataba mifupi.
Mwanaspoti linafahamu Simba wapo katika mazungumzo na TFF kuomba nafasi ya kuwatumia pia katika ligi na mashindano mengine ya ndani wachezaji ambao watawasajili kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndio maana hawajatangaza usajili wa Lokosa.
Mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema mpaka Simba wamefikia uamuzi wa kutaka kumleta Kone, basi kuna mambo ambayo ya kiufundi wameyaona kwake na akiongezeka katika kikosi ataifanya timu hiyo kuwa bora katika eneo la katikati. “Simba ambacho wanatakiwa kukifikiria wakati huu ni kufanya usajili wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kuna ushindani wa kweli na wachezaji wa maana wenye viwango vya juu na si mashindano ya ndani ambayo timu yao ina kikosi cha kushindana na kufanya vizuri,” alisema Ulimboka ambaye ni miongoni mwa mastaa wa zamani wenye mapenzi na Simba.
Kwa mujibu wa takwimu za Simba, Kone amezaliwa Desemba 19, 1990 na nafasi ambayo anacheza ni kiungo mkabaji au mshambuliaji ambapo alianza kucheza soka la ushindani 2014 katika timu ya AS Real Bamako, 2014-15 akacheza MAS Fez baada ya hapo 2016-17 akaenda Al - Oruba na mwaka 2017 alijiunga na Stade Malien.
Simba wanaamini kwamba kwa kiwango cha Kone anaweza kuwa mshindani wa Mkude ambaye amesimamishwa kwa muda na uongozi kwa sababu za kinidhamu