Balozi wa Marekani nchini Uganda Natalie E. Brown amezuiliwa na maafisa wa usalama kwenda kumtembelea nyumbani kwake kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulani ambaye pia ni mwanamuziki Bobi Wine, Januari 18.
Balozi huyo alikuwa anatekeleza jukumu lake ambapo Marekani mara kwa mara hukutana na wadau mbalimbali wa kisiasa nchini Uganda kama sehemu ya shughuli zake za kidiplomasia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ubalozi huo wa Marekani:
‘’Lengo la balozi Brown lilikuwa ni kuangalia afya na usalama wa Bobi Wine hasa ikizingatia kwamba hajaruhusiwa kutoka nyumbani tangu uchaguzi huku maafisa wa usalama wakiwa wamezingira nyumba yake.
Taarifa hiyo inaendelea kudai kuwa kampeni za uchaguzi Uganda zilikumbwa na unyanyasaji wa wagombea wa upinzani, waendesha kampeni na wafuasi wao pamoja na kukandamizwa kwa vyombo vya habari na shughuli zinzoendeshwa na mashirika ya kijamii, na kufungwa kwa intaneti kabla ya baada ya uchaguzi.
Taarifa hiyo imesema hatua hizo zisizokubalika kisheria na kifungo cha nyumbani kwa mgombea urais kunaendeleza wasiwasi juu ya demokrasia ya Uganda.
‘’Tunatoa wito kwa serikali ya Uganda kuheshimu haki za raia wake na uhuru wa msingi, ikiwemo uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru kwa vyombo vya habari kama ilivyo katika katiba ya Uganda na kulingana na kujitolea kwa Uganda kuendeleza haki za binadamu.’’
Ubalozi wa Marekani unasema hakuna yeyote anayestahili kunyimwa uhuru wa kuwasiliana na uhuru wa kuondoka nyumbani kwake anapotaka kufanya hivyo.