KLABU ya Simba jana ilipata Mwenyekiti wao mpya baada ya Murtaza Mangungu kushinda kwenye uchaguzi mdogo kwa kumbwaga Juma Nkamia na kuanika mambo 11 ambayo atayapa kipaumbele kwenye kipindi chake cha uongozi ndani ya klabu hiyo.
Mangungu alishinda kwa kishindo jana kwa kupata kura 802 kati ya 1140 zilizopigwa kwenye uchaguzi mdogo wa klabu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ushindi wa asilimia 70.35 dhidi ya kura 330 alizopata Nkamia ambazo ni sawa na asilimia 28.95.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, Boniface Lihamwike ndiye aliyemtangaza Mangungu kuwa mwenyekiti mpya wa klabu hiyo akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Swedy Nkwabi aliyejiuzulu ghafla Septemba mwaka juzi na nafasi yake kukaimiwa na Mwina Kaduguda tangu Novemba mwaka huo kabla ya kuitishwa uchaguzi huo uliomuingiza mwenyekiti huyo mpya.
“Waliopiga kura ni wanachama 1140, kura nane zimeharibika na Juma Nkamia amepata kura 330 sawa na asilimia 28.95,” alisema Lihamwike jana akitangaza matokeo ya uchaguzi huo.
Baada ya ushindi huo, Mangungu alizungumza na gazeti hili na kueleza kwamba katika uongozi wake atayapa kipaumbele mambo 11. Moja ya mambo hayo ni klabu kuwa na akademia na mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.
“Siwezi kuyataja yote kwa wakati huu, lakini katika uongozi wangu na mambo 11 nitakayoyapa kipaumbele, ikuwamo ili la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ambalo ni suala la kisheria.