Dodoma. Mabingwa wa soka nchini, Simba, wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, wakati kiungo wake, Benard Morrison akitoa pasi ya bao na kufunga la ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini hapa.
Morrison aliifungia Simba bao la ushindi kipindi cha pili baada ya kutoa pasi ya bao la kwanza wakati, kipindi cha kwanza kikimalizika kwa sare ya 1-1.
Wakati Simba ikizidi kuisogelea Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, KMC ilitumia vizuri Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC.
KMC imeanza kunufaika na usajili wao wa dirisha dogo baada ya Charles Ilanfya na Matheo Anthony waliosajiliwa sasa kuingia katika kitabu cha wafungaji.
Jijini Dodoma, ushindi wa Simba umeonekana kuwa na dalili nzuri kwa kocha mpya wa mabingwa hao watetezi, Didier Gomez, ambaye ndiyo mchezo wake wa kwanza kusimama kama kocha katika ligi.