MFARANSA wa Simba, Didier Gomes amewaambia wachezaji kwamba hataki mbwembwe nyingi za ‘anao anao’ yeye ni ‘unagusa unaachia twende’.
Gomes amesisitiza kwamba kikubwa anachotaka kwenye timu yake ni mpira wa kasi unaovutia na ushindi mnono.
Kocha huyo aliyetua Simba akitokea El Merreikh ya Sudan ambayo wapo nayo kundi moja la Ligi ya Mabingwa, ameapa kwamba kama wachezaji wakizoeana vizuri na kuelewa staili yake ya uchezaji timu zitapigwa nyingi.
Lakini amefurahishwa pia na ubora wa Bernard Morrison ambaye juzi alimpa dakika 25 akatupia bao mbili kwenye mechi dhidi ya Al Hilal.
Alisema anapenda soka la kumiliki mpira muda mwingi na kutengeneza nafasi za kufunga, huku akitaka wachezaji waongeze zaidi bidii mazoezini kuwa fiti kumudu kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwenye mechi yake na Al Hilal ya Sudan ambayo ni mtani wa El Merreikh alisema: “Niliamua kuanza na mfumo wangu wa 4-4-2, ambao Parfect Chikwende kucheza nyuma ya straika Meddie Kagere ili kuwa na uwezo wa kufunga muda wowote, lakini nyuma yao kuwa na wachezaji wengine wanne Clatous Chama, Larry Bwalya, Francis Kahata na Taddeo Lwanga ili kutawala na kumiliki mpira.