Wakati kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa akisema kuwa atayatumia mashindano ya Simba Super Cup kuwajua vizuri wachezaji wake huku kocha wa Al Hilal ya Sudan,Zoran Manojlovic akitamba kuwa ana kikosi bora kitakacholeta ushindani katika michuano hiyo.
Simba itafungua pazia la michuano hiyo kwa kucheza na Al Hilal kesho kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa na tayari wapinzani wao wamewasili Tanzania leo mchana tayari kwa mashindano hayo yanayoshirikisha timu tatu ikiwemo wenyeji Simba, Al Hila na TP Mazembe ya Congo.
Gomes amesema wanatakiwa kupambana na kushinda kila mechi ili kujiongezea kujiamini wakati huu wanapojiandaa na mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Katika mashindano hayo itakuwa nafasi kwangu kuwaona wachezaji na kujua uwezo wao na kuandaa mfumo mzuri kwa ajili ya mechi za Ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika ," amesema Gomes .
Kocha wa Al Hilal,Zoran Manojlovic amesema kuwa wamekuja kushindana wakiamini kuwa atatoa ushindani mzuri kwa wapinzani wao ambao wanayatumia mashindano hayo ujiandaa na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Tunashukuru tumefika salama licha ya safari ngumu tangu jana.Tumejipanga vizuri tukiwa tayari kwa ajili ya mashindano hayo ambayo yanashirikisha timu kubwa na tunaamini tutawapa maandalizi mazuri katika mashindano yao yanayowakabili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ,"alisema Manojlovic
Naye nahodha wa timu hiyo, Abdellatif Saeed amesema wamekuja katika michuano hiyo kushindani na anaamini watafanya vizuri na kutwaa ubingwa.
Simba, Al Hilal kamili Super Cup
