Siku 24 baada ya kutoka taarifa ya Uongozi wa klabu ya Simba kumsimamisha mchezaji wao nyota, Jonas Mkude hatimaye amejitokeza hadharani na kuomba radhi.
Taarifa ya kusimamishwa Mkude ilitoka Desemba 28 mwaka jana kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Baada ya taarifa hiyo Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alilizungumzia sakata hilo kuwa bado linaendelea kwenye hatua kinidhamu na taarifa itatoka.
Leo Januari 21, Mkude kupitia akaunti yake binafsi ya Instagram ameomba radhi na kusema kuna mambo yalitokeza baina yake na Uongozi wa Simba.
"Naomba radhi kwa wachezaji, wanachama, mashabiki, benchi la ufundi na uongozi wanisamehe, kwasababu binadamu yoyote anakosea. Nachowaahidi jambo hili halitatokea tena," amesema Mkude
Mkude amekuwa kiungo muhimu kwenye klabu hiyo amekosa michezo kadhaa ukiwemo wa kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.