KUTOKANA na kasi aliyonayo winga wa Yanga, Mkongomani Tuisila Kisinda ‘TK Master’ zimemtikisa beki wa zamani wa kimataifa wa Simba, Boniface Pawasa aliyeamua kutoa mchongo kwa mabeki wa timu pinzani kuweza kumdhibiti na kuondokana na presha kubwa.
Tuisila aliyesajiliwa msimu huu kutoka AS Vita ya DR Congo, amekuwa akisifika kwa kasi kubwa na hasa kuwapora mipira na kuwatoka mabeki, ikiwamo kitendo alichomfanyia beki wa Simba, Joash Onyango katika Kariakoo Derby na kusababisha kumchezea faulo iliyozaa penalti.
Penalti hiyo ilitumiwa vyema na Yanga kujipatia bao lao kupita Michael Sarpong kabla ya beki huyo kutoka Kenya kusahihisha makosa kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za lala salama na kufanya matokeo ya mchezo huo uliopigwa Novemba kumalizika kwa sare ya 1-1.
Hata hivyo, kwa uzoefu alionao katika nafasi ya beki, Pawasa aliiambia Mwanaspoti amekuwa akimfuatilia winga huyo wa Yanga na kubaini mbinu ambazo mabeki wa timu nyingine wanaweza kuzitumia ili kumdhibibiti uwanjani.
Pawasa alikiri Tuisila ni mchezaji hatari ambaye hatakiwi kupewa nafasi ya kumiliki na kuvuta mpira kisha kugeuka na kuanza kukimbia nao, badala yake mabeki wacheze kwa kumkaba mtu kwa mtu.
Alisema Tuisila ni mchezaji anayetumia akili kubwa, kwamba akimaliza jambo lake la kuwapa presha mabeki, kisha anaanza kutembea kama vile hayupo uwanjani, kitu alichokigundua kinawasahaulisha mabeki wasijue anavuta pumzi ya kuweka mwili wake upya kwa ajili ya kuwasumbua zaidi.
“Tuisila hatakiwi kupewa nafasi, beki namba mbili na beki wa kati ndio wanapaswa kuwasiliana namna ya kumkabili, ndipo wanaweza wakapunguza makali yake, kwani si mchezaji ambaye anaingia ndani ya eneo la penalti, huwa anakimbilia pembeni hiyo ndio nafuu yao, lasivyo angekuwa anawaliza mara kwa mara,” alisema Pawasa ambaye kwa sasa ni kocha na kuongeza;
“Tuisila hafikii mbio alizokuwa nazo Said Maulid ‘SMG’ wakati wa kumkaba, tukiona mpira umepigwa kwake, mmoja anabaki nyuma, mwingine anaenda kukabana naye bila kumwachia nafasi, mbaya zaidi alikuwa anamlazimisha beki amfanyie makosa ndani ya eneo la penalti, ndio maana jina lake lina nguvu hadi leo, kitu ambacho Tuisila anakikosa.”
Alimshauri Kocha Cedric Kaze kumuongezea maarifa Kisinda kwamba anapokokota mipira awe anaangukia ndani ya eneo la penalti na sio nje, ili kushinda mbinu za mabeki wajanja wanaokuwa wanamvutia nje na timu kuishia kupata faulo ambazo ni mara chache wakafunga.
“Laiti Tuisila angekuwa ananyanyua macho yake kuona anaenda wapi angekuwa hatari zaidi, pia awe anaangukia ndani ya eneo la penalti na sio anavyofanya kutumia nguvu nyingi, wakati mwingine haziifaidishi timu, ila ni mchezaji mzuri sana anayetakiwa kuonge-zewa maarifa kidogo sana,” alisema.
Naye nyota wa zamani wa Simba, aliyewahi kuzinoa timu kadhaa nchini ikiwamo Kagera Sugar, Njombe Jiji na Lipuli ya Iringa, Mrage Kabange, alisema Tuisilada ni mchezaji anayetakiwa beki asilale pindi anapokuwa na mpira, kisha asimruhusu aukokote mbele yake.