Mwanzilishi wa kampuni ya Amazon Jeff Bezos amejiuzulu katika wadhifa wake wa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ya biashara ya mtandaoni ambayo ilianza katika gereji yake karibu miaka 30 iliyopita.

Bwana Bezos sasa hivi atakuwa mwenyekiti, hatua aliyosema itampa “muda na nguvu zaidi” kuangazia biashara zake zingine.
Nafasi ya Bwana Bezos, ambaye ni miongoni mwa wanaume tajiri zaidi duniani, itachukuliwa na Andy Jassy, ambaye sasa hivi anaongoza biashara ya uhifadhi wa data.
Mabadiliko hayo yatafanyika katika kipindi cha nusu ya pili cha mwaka 2021, taarifa kutoka kampuni hiyo imesema.
“Kuwa Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Amazon ni majukumu muhimu na yenye kuhitaji muda. Ukiwa na jukumu kama hilo. Ni vigumu sana kutoa angalizo kwa mambo mengine,” Bwana Bezos amesema katika barua aliyoituma kwa wafanyakazi wa kampuni ya Amazon siku ya Jumanne.
“Kama mwenyekiti nitakuwa najihusisha na mambo mengine muhimu ya kampuni ya Amazon lakini pia nitakuwa na muda na nguvu ya kuangazia miradi ya Day 1 Fund, Bezos Earth Fund, Blue Origin, The Washington Post, na mingine ninayotaka kuikuza zaidi.”
“Sikuwa na nguvu inayohitajika lakini hilo halina uhusiano wowote na kustaafu. Nina shauku kubwa juu ya kile ambacho nafikiria kuwa kinaweza kutimizwa na kampuni hii,” aliongeza.
Bwana Bezos anaangaziwa sana na umma
Bwana Bezos, 57, ameongeza kuwa kampuni ya Amazon tangu ilipoanza biashara ya uuzaji wa vitabu mtandaoni 1994.
Kampuni hiyo yenye wafanyakazi milioni 1.3 kote duniani na yenye kujihusisha na karibu kila kitu kuanzia kufungasha kwa bidhaa, huduma za video, uhifadhi wa data na biashara.
Bwana Bezos anadaiwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 196.2, kwa mujibu wa orodha ya mabilionea wa jarida la Forbes.
Kampuni hiyo iliendelea kuimarika zaidi mwaka jana wakati janga la corona lililopokuwa linaendelea kusambaa na kusababisha kuongezeka kwa manunuzi ya mtandaoni.
Kampuni hiyo iliripoti kufanya mauzo ya dola billioni 386 mwaka 2020, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 tangu mwaka 2019.
Faida iliongezeka karibia mara dufu hadi dola bilioni 21.3.
Akitangaza mipango yake, Bwana Bezos alisema ataendelea kuangazia zaidi bidhaa mpya na miradi aliyokuwa ameitilia nia mapema.
“Ukiangalia matokeo yetu kifedha, kile hasa kinachoonekana ni matokeo ya ubunifu wa muda mrefu,” amesema. “Sasa naiona Amazon katika kipindi cha ubunifu kuliko wakati mwingine wowote ule, na kufanya kuwa wakati muafaka wa mabadiliko haya.”
Mabadiliko hayo yanawadia wakati ambapo Bwana Bezos anaangaziwa sana na umma.
Ametalakiana na mke wake, wanaharakati wa wafanyakazi na wanaopigania usawa wanamuandama huku akiangazia biashara zingine kama vile ya kutaka kujenga mazingira ya kuishi katika anga la mbali ya kampuni ya Blue Origin na gazeti za Washington Post.
‘Bezos hajiondoi katika kampuni ya Amazon‘
Kampuni ya Amazon pia inafuatiliwa kwa karibu na wadhibiti, kwa shutuma za ukiritimba. Na utawala wake katika biashara ya uhifadhi wa data inapata changamoto kutoka kwa kampuni zingine kama vile Microsoft and Alphabet, kampuni mama ya Google na YouTube.
Uamuzi wa Bwana Bezos kuachilia majukumu ya kila siku ya kampuni yake haikuwa inatarajiwa ingawa haikushangaza wawekezaji na pia ilikuwa na athari ndogo sana katika bei ya hisa za kampuni hiyo saa za baadaye.
Katika wito kutoka kwa wachambuzi wa kujadili masuala ya fedha ya kampuni hiyo, Afisa mkuu wa fedha wa Amazon, Brian Olsavsky amesema: “Jeff hajiondoi kwenye kampuni hii, anaanza kazi mpya… Bodi inajishughulisha kweli na pia ni muhimu sana katika mafanikio ya kampuni ya Amazon.”
Bwana Jassy, aliyehitimu katika chuo kikuu cha Harvard, amekuwa akifanyakazi na kampuni ya Amazon tangu mwaka 1997 na pia amesaidia katika ubunifu wa huduma mtandaoni zinazotolewa na kampuni ya Amazon, ambazo kwa muda mrefu zimeonekana kama kuwa kichocheo kizuri cha mafanikio ya kampuni hiyo.
Andy anafahamika vyema katika kampuni hiyo na amekuwa katika kampuni ya Amazon sawa na kipindi ambacho pia mimi nimekuwa kwenye kampuni hii.
Atakuwa kiongozi mzuri na nina imani naye kabisa,” Bwana Bezos amesema.