Waandaji wa tuzo za muziki za MTV Mama 2021 wamemtaja msanii Diamond Platnumz kuwa Mtanzania pekee atakayetumbuiza kwenye tamasha hilo.
Taarifa hiyo ni sawa na kusema MTV wameingia kwenye kumi na nane za Diamond Platnumz kwa sababu mwaka jana walimpa fursa kama hiyo na akaandika historia.
Ilikuwa hivi, mwaka jana, kampuni ya MTV Networks Africa iliandaa tamasha kwa ajili ya kuchangisha pesa za kusaidia familia zilizoathirika na matokeo ya janga la corona. Tamasha hilo lililopewa jina la Africa Day Benefit Concert lilikusanya zaidi ya wasanii wakubwa 30 wa Afrika kwa ajili ya kutumbuiza.
Hata hivyo, kwa sababu ya corona utumbuziaji ulifanyika kwa njia ya mtandao. Yaani wasanii walikuwa wanatumbuiza kutokea nyumbani, kisha video zao zinaonywesha kupitia akaunti ya Youtube ya MTV Africa.
Katika tamasha hilo hakukuwa na cha Burna Boy, Davido wala Wizkid, wote walifunikwa na shoo kali na ya kipekee aliyoifanya Diamond kiasi kwamba mpaka alichaguliwa kushindania tuzo ya watumbuizaji bora wa kipindi cha corona.
Aidha majina ya wasanii nane yaliyojitokeza kwenye orodha ya watumbuizaji kwenye tuzo za MTV Mama mwezi Februari ni Diamond (Tanzania), Nasty C (Afrika Kusini), Soraia Ramos (Cape Verde), Khaligraph Jones (Kenya), Sheeba (Uganda), WizKid (Nigeria), Suspect 95 (Ivory Coast) na kundi la Calema kutoka Sao Tome.