KITENDO cha kocha Yanga, Cedrick Kaze kuwatimua nyota wake waliochelewa mazoezini kinadaiwa kuzua jambo huko Jangwani huku wadau wakichelekea kwa kusema yalikuwa maamuzi sahihi na walipaswa kupigwa faini.
Mastaa wa Yanga akiwemo Mukoko Tonombe walijikuta wakijaa kwenye kumi na nane za Kaze baada ya kuchelewa mazoezini, wakitoka mapumziko waliyopewa ya siku 10 yakiwa na sharti la kuwahi kuripoti.
Wachezaji wote wa Yanga walitakiwa saa 6:30 mchana wawe ndani ya geti la kambi yao iliyopo kule Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mukoko, Haruna Niyonzima, Carlos Guimaraes ‘Carlinhos’, na kipa Farouk Shikhalo walichelewa na kurudishwa walipotoka lakini jambo hilo lilimalizwa na kurejeshwa ka mbini kuungana na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezaji pekee aliyechelewa na kuruhusiwa kuingia alikuwa beki mpya wa timu hiyo, Dickson Job ambaye aliwasili kambini hapo kuanza kazi na alikuwa haelewi taratibu za Kaze.