Dar es Salaam. Kutolewa kwa Taifa Stars kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) kumeibua mjadala. Taifa Stars ilimaliza mchezo wake wa Kundi D juzi, kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Guinea na kufikisha pointi nne, amnazo zilishindwa kuwazidi Zambia na Guinea. Ushindi pekee ungeweza kuivusha timu hiyo ya kocha Etienne Ndayiragije katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayoendelea nchini Cameroon. Awali timu hiyo ilichapwa na Zambia mabao 2-0 na kuifunga Namibia bao 1-0 kwenye mchezo wa pili wa kundi lake, ambao uliamsha matumaini ya kufanya vizuri msimu huu. Matokeo hayo sasa yanalingana na yale ya 2009, wakati Taifa Stars iliposhiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo, ambako pia ilimaliza ikiwa na pointi nne, ikitakiwa kushinda katika mchezo wa mwisho, badala yake ikalazimishwa sare za Zambia. Wachezaji wa zamani pamoja na makocha ambao waliutazama mchezo huo muhimu wa mwisho na ushiriki wa Taifa Stars kwa ujumla, walisema uchaguzi wa kikosi, mpango wa mechi na nidhamu ya mchezo vilichangia kukosa pointi tatu za juzi. Kocha Amri Said alisema Stars imeondoshwa baada ya kukosa mbinu za kujilinda ilipofunga bao la pili, kauli sawa na iliyotolewa na Mtemi Ramadhan. “Tulipopata bao la pili lilituvuruga na likawaongezea presha Guinea, lakini tulikosa mbinu za kulinda, pale ndipo tulipotakiwa kubadili kabisa mbinu zetu,” alisema Mtemi Ramadhan. Nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars, Simba na CDA ya Dodoma, alisema pamoja na kwamba Guinea si timu mbovu, lakini Stars ilikuwa na nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali, japo ilikosa misingi ya mpira kulinganisha na wapinzani wao. “Walikuwa wanapiga tu mipira mbele wakiamini bao linakuja, wapinzani wao walitafuta bao kwa kutumia njia sahihi za mpira, hicho ndicho kilitugharimu. “Lakini naamini watu wengi watamlaumu kocha kwa wachezaji aliowaacha, lakini mimi niko tofauti kidogo, nampongeza kwa kuwajumuisha chipukizi kikosini na hakuogopa kuwatumia, kama ataendelea kuwapa nafasi naamini watafanya vizuri,” aliongeza. Amri Said alisema ukomavu wa soka uliwasaidia Guinea, alisema: “Kabla ya kufungana, tuliona kipa wao alivyokuwa na mbinu za kimpira, sisi tulipaswa kutumia mbinu ya kujilinda baada ya kuongoza 2-1, lakini kocha hakufanya hivyo,” alisema. Mohammed Kiganja, katibu mkuu wa zamani wa BMT, alisema kocha alipaswa kutumia mbinu ya kujilinda baada ya kupata bao la kuongoza. “Nilishangaa hata kipa wetu hakuwa na mbinu ya kupoteza muda hata kwa kudanganya kaumia ili kuipa timu nafasi ya kujipanga, lakini hakufanya hivyo,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa baraza la michezo (BMT).
Nidhamu ya kujilinda imeitoa Stars
